Njama na Hila za Ulanguzi/Utapeli

Kisa cha kuandika makala hii si kuwafanya wazalendo waishi kwa hofu, hapana, na wala sitaki kujifanya eti mimi mjanja sana, bali imedhihirika kwamba bado kuna watu ambao hawazijui njama na hila zote za walanguzi au matapeli wa hapa Ujerumani, kutumia simu na intaneti. Habari hizi ni kuwafahamisha wananchi kwa ujumla na kuwasaidia wale wanaoandamwa na wahalifu (chakula ya fisi). Kitambo rafiki yangu mmoja (Mjerumani) alinyolewa EUR 500 (ni kiasi kidogo ukilinganisha na maelfu waliyonyolewa watu wengine!). Walanguzi au matapeli wengine sana sana wanajaribu kuwalangua wageni  wengi (yaani watu wasio Wajerumani). Wanaangalia kwenye CD-ROM za simu na midia nyingine, wanaulizia posta, halafu wanatafuta majina gani ni ya kigeni ili wajaribu kuwalangua au kuwatapeli watu hao. Walanguzi au matapeli wenyewe (chakula ya fisi) wanafikiri kwamba wageni ni watu wajinga na saa zote huwa na   watoto elfu kidogo, ambao wanaweza kulanguliwa kirahisi. Zifuatazo ni njama kadhaa tu kati ya njama chungu nzima/mbovu.

Simu na SMS

Kwanza: (1) Mtu (mara nyingi ni   mwanamke) anapiga simu kwako au kukutumia SMS na kuacha ujumbe eti umpigie simu. Kumbe namba ya simu yake ni moja kati ya zile za bei ya kuruka. Kwa wenye Handy pia kuna kitu kiitwacho "Fangschaltung" ambapo hata ukikata simu, hela zako zinaendelea kulika kwa muda usiopungua saa nzima!!! Ingawa watu wanazijua namba zinazoanzia 0190 au 0900 lakini wengine hawajui kwamba siku hizi kuna  nyingine pia ambazo ni hatari au za kitapeli, kwa mfano 0137, 0136, 118, 0193, 01033, 0180 n.k. na kila siku zinazidi kuongezeka. Ingawa namba zenyewe zinajulikana, lakini saa zingine huandikwa kinamna ili zisibainike kirahisi. Kwa mfano 0137 inaweza kuandikwa +4913777767 au (49)+13-77-88-13 au 01013-7778... Kwa watu wanaoandamwa, ukiachiwa ujumbe na mtu usiyemjua, ni bora kutopiga simu kabisa. Ikilazimu basi piga simu kwenye kibanda cha simu na sio kutoka nyumbani, kwani kwenye kibanda utaona hela zako zinavyolika. Ujumbe wenyewe unaweza kuwa kwa SMS, simu au kadi katika sanduku lako la barua (kwa mfano ikisema eti kuna kifurushi chako). Pia siku hizi kuna namba za matapeli ambazo hazina kodi (yaani "Vorwahl") ya kitapeli. Kwa hiyo hazibainiki kirahisi.

Pili: (2) Mtu (karibu saa zote ni mwanamke au kaseti/kanda inachezwa) anapiga simu kwako na kusema kwa haraka sana eti umeshinda zawadi au kuna ujumbe wako au kitu kingine cha upuuzi, na kwamba ukitaka kuusikiliza ujumbe huo, ubonyeze namba fulani kwenye simu yako. Hapo utaingia kwenyebei ya kuruka. Ingawa mtu mzima atajua kwamba huu ni mtego, mtoto je? Walanguzi hao hujaribu kupiga simu saa za kazi wakitumai kwamba watoto wako nyumbani peke yao bila wazazi. Akipokea simu mtu mzima, basi walanguzi hao hawasemi kitu au wanasema wamekosea namba. Walanguzi wengine hujaribu kujua kama kuna watoto nyumbani kwako. Basi hujidai eti wanafanya kura ya maoni, yaani "Umfrage" kuhusu watu walio na umri chini ya miaka 29 au upuuzi mwingine. Hakuna "Umfrage" yo yote ambayo hufanyika kwa simu, kwa hiyo usijibu maswali yo yote, bali ni vizuri kuwa mkali papo hapo na kumwambia kwamba unarekodi sauti yake.  Dawa ya kwanza: Mtu kama huyo ni kumwambia kwamba umeandika namba yake ya simu, unarekodi sauti yake, unajua njama zote za walanguzi na kama kuna watoto, watoto wote wameambiwa kwamba wakiambiwa wabonyeze namba fulani, wakate simu papo hapo. Halafu mtukane na kumwambia akipiga simu tena atafunguliwa mashtaka. Dawa ya pili: Jambo la maana ni kwenda posta na kuomba  wafunge  ("sperren") namba zote za kijangili, yaani 0190, 0900, 0137 n.k. zisiingie wala zisitoke kwako. Huduma hii inagharimu EUR 7,50 mara moja tu. Lakini hii inasaidia kiasi fulani tu, kwani walanguzi wanaweza kukuvamia kupitia mlango wa uani. Kwa mfano wanaweza kupitia 010... na kuingia 0190 au 0900. Kinga kabambe kabisa inagharimu kama EUR 5 au 10 kwa mwezi (kwa mfano DSL). Katika duka la T-Online watawaelezeni zaidi.

Faksi

Mtu anatumiwa faksi za kishenzi nyingi nyingi tu kila siku. Kwenye faksi hizo hakuna anwani wala jina la kampuni ila kuna "Faxabruf" tu, na namba zenyewe ni za bei ya kuruka. Kwa hiyo mtu hawezi kujihami. Halafu mtu anaambiwa eti akitaka asitumiwe faksi zingine, basi apige simu fulani. Simu hiyo ni ya bei ya kuruka, na hata ukipiga simu utaendelea kupata faksi za kishenzi ili upige simu tena. Kuna mtu mmoja ambaye amejitolea mhanga na anatoa mawaidha jinsi ya kutatua tatizo hili.
Yuko www.optimasoftware.de Jambo la maana ni kutowapa watu unaowashuku au usiowajua, namba yako ya faksi, bila sababu maalum. Ikiwezekana, pia hakikisha kuwa namba yako ya faksi haijaandikwa po pote kwenye Intaneti. Vile vile epukana kabisa na "Fax-Abruf"

Intaneti

Siku hizi kila mtu anajua kwamba zile "dialer" saa zote zinataka mtu abonyeze kitu fulani au kibonye fulani au ajaribu kufunga "pop-up". Usije ukalogwa kubonyeza "OK", "dieses Fenster schließen" au ile "x" iliyoko juu kulia au upuuzi mwingine wo wote. Vizuri ni kutoigusa pop-up kabisa (hata kama imefichwa kwenye boksi au fremu). Ikibidi, basi pop-up hufungwa kutumia   "Alt F4" au "Str+Alt+Entf". Halafu "Task beenden". Lakini saa zingine programu hizo zinaweza kuwekwa kwenye kompyuta yako bila wewe kubonyeza kitu. Kwa mfano mtu ukikosea kuandika anwani na kujikuta kwenye tovuti (Website) mbovu au chafu au kwa wale wanaopenda kutembelea saiti mbovu au za uchafu. Pia ni vizuri kufahamu kuwa wahalifu wanaweza "ku-deactivate" au kuipenya "firewall" yako. Kwa hiyo uwe unaichunguza mara kwa mara. Kwa wasio na uzoefu wa mtandao, usije ukalogwa kufungua E-mail inayotoka kwa mtu usiyemfahamu, au inayotoka kwa mtu unayemfahamu, lakini kichwa cha habari ("Betreffzeile") hakiko vilivyo. Hata hivyo, siku hizi ukiletewa bili iliyopita kiasi, unaruhusiwa kukataa kuilipa na kuanzisha ubishi hata mahakamani. Pia ukiletewa imeili eti kutoka benki yako au shirika lingine linalokushughulikia, ikisema kwamba eti u-update mambo yako   "Ihre Angaben aktualisieren" kwa mfano anwani yako, neno lako la siri "Passwort", namba ya "credit card" n.k. usije ukalogwa kujaza fomu yo yote kwenye mtandao/Internet. Barua pepe (imeili) nyingi za namna hiyo hutumwa na walanguzi wanaotaka kukuibia hela. Kama benki yako au shirika lako wanataka anwani yako mpya n.k. basi uwapigie simu na kuwaambia kwamba utawatumia maelezo hayo kwa barua au utakwenda mwenyewe kwao.

Mwisho

Kama umegundua njama au hila nyingine mpya, basi unaweza kutuandikia na tutaiandika hapa ili wazalendo wote wajue, kwani walanguzi saa zote wanagundua njama na hila mpya za kuwalangua watu.Kaeni chonjo!!! Habari zaidi ziko kwa mfano: Bundesamt für Sicherheit in der Informationstechnik Habari zingine ziko kwenye viungo vilivyoko kwenye ukurasa wa "links" wa saiti hii.